KILIMO CHA TIKITI MAJI( WATER MELONY)

 


Leo tunakwenda kujifunza jambo muhimu sana ambalo wakulima wengi wa tikiti maji hua hawalifahamu au kama wanalifahamu hawalifahamu kwa kina ipasavyo. Ikumbukwe kwamba Hata ijapokua utafanya vizuri shughuli za shamba, kuna kigezo kikuu cha uzalishaji wa matikiti maji, ambacho kama usipokifahamu unaweza kupata hasara hata kama kila kitu umejitahidi kukifanya vizuri. Kigezo hicho ni UCHAVUSHAJI au kwa kitaalamu huitwa Pollination. Uchavushaji katika matikiti maji ni kigezo kikuu katika uzalishaji kitakachoamua wingi wa mavuno yako. Kwenye kilimo cha tikiti, Uchavushaji na utengenezaji wa Matunda ni sekta nyeti sana inayohitaji uangalizi  wa hali ya juu. Ili kuelewa hili vizuri  tutajifunza kidogo sayansi ya utengenezwaji wa maua ya mmea wa tikiti maji. Kwanza tuanze na kufahamu maana ya Uchavushaji. Karibu sana darasani.

UCHAVUSHAJI (POLLINATION)

Uchavushaji ni urutubishaji wa ua la kike la mmea kwa kutumia poleni (mbegu ya kiume) kutoka kwenye sehemu ya kiume ya ua la kiume. Mchakato huu wa uchavushaji ndio hupelekea utengenezaji wa tunda.

Utengenezwaji wa Maua

Kila mkulima anapaswa kufahamu namna/jinsi maua ya tikiti maji yanavyotengenezwa ili kupata uelewa wa utaratibu wa uchavushaji unavyofanyika. Mmea wa tikiti una maua ya kike na maua ya kiume. Tikiti linapofikia hatua ya kutoa maua, maua ya kiume hutoka kwanza na maua ya kike hutokeza baadaye, na kwa kawaida maua ya kiume ni mengi kuliko maua ya kike. Hivyo unapoona maua mengi kwenye tikiti usidhani yote yatatengeneza matunda, asilimia kubwa sana ya maua pale ni maua ya kiume, ambayo kazi yake kubwa ni kutoa poleni (mbegu) kwa ajili ya kuchavusha maua ya kike. Ua la kike lina maisha mafupi (short lifespan), linaishi kwa siku moja tu, yaani mara linapofunguka ua la kike linaweza kua hai kwa ajili ya kurutubishwa kwa siku hiyo moja tu. Siku moja inapoisha kama Ua hilo la kike halijapata poleni kutoka ua la kiume kwa ajili ya kufanya uchavushaji basi ujue tunda halitatengenezwa na ua hilo la kike litaharibika. Kama tulivyoona kwamba Mmea wa tikiti unakua na maua mengi ya kiume kuliko ya kike, hii ina maana kwamba mmea unatoa maua mengi ya kiume ili kwamba ua la kike linapotengenezwa na kufunguka likute tayari kuna maua ya kiume yenye poleni ili kurahisisha uchavushaji. Sasa changamoto hapa ni namna ya kuhamisha poleni kutoka maua ya kiume kwenda kwenye ua la kike kabla halijapoteza uhai wake.

Idadi ya matunda katika mmea wa tikiti inategemea mambo yafuatayo:

Aina ya mbegu (variety).

Hali ya hewa

Rutuba ya udongo

Umwagiliaji (maji)

Idadi ya wkala wa uchavushaji (pollination agent)

Mambo muhimu ya Kuzingatia

Matikiti maji yanahitaji wadudu kwa ajili ya kufanya uchavushaji. Ua la kike lazima litembelewe na mdudu angalau mara saba ili kutengeneza tunda lenye ubora.
Uchavushaji usiokidhi/usiotosheleza (insufficient pollination) hupelekea matunda yenye muundo usiofaa (misshapen) ambayo ni hasara kubwa kwa mkulima. Mfano Unakuta tunda kwenye kitako (mwisho) ni nene na hapo mwanzoni karibia na kikonyo ni jembamba. Hii ina maana kwamba poleni haikutosheleza hivyo haikufika hadi mwisho kwenye kikonyo..
Idadi ya nyuki ndiyo huamua ubora wa uchavushaji (pollination). Nyuki ndio wakala mkuu wa uchavushaji kwenye matikiti, hivyo mkulima anapaswa kuweka mizinga ya nyuki shambani kwake ili kuwezesha uchavushaji
Kama Mkulima hataweza kuweka mizinga ya nyuki, basi aweke maji maeneo mbalimbali ya shamba
ili kuvutia wadudu wakiwamo nyuki kwa ajili ya kusaidia uchavushaji. Unaweza kuchimba vidimbwi vya wastani na kuhakikisha vinakua na maji wakati wote, tangu maua yanapoanza kutengenezwa.
Tumia dawa za kuvutia nyuki (bee addicts). Bee addicts huvutia nyuki wengi sana shambani mwako.
Haribu au ondoa mimea yote ambayo inatoa maua ambayo iko shambani mwako au pembeni ya shamba lako. Mfano magugu yanapoachwa hadi kutoa maua husababisha nyuki kutembelea maua ya magugu au mimea mingine na kuacha au kupunguza kutembelea mimea ya matikiti. Hii ni kwasababu moja kubwa kwamba, maua ya tikiti hayavutii nyuki (hayana mvuto kivile kwa nyuki), yaani nyuki atatembelea maua ya tikiti endapo patakua hakuna maua mengine maeneo hayo au jirani ya shamba lako. Hivyo basi kuondoa mimea mingine yenye kutoa maua na kubakiza matikiti peke yake kutahakikisha nyuki wanafanyia kazi maua ya tikiti tu.
Epuka kupiga dawa za wadudu na magonjwa (insecticides and fungicides) kipindi hichi cha uchavushaji maana dawa hizi zinaweza kuua nyuki (hususani dawa za wadudu) au kuwazuia washindwe kufanya majukumu yao ipasavyo. Kama patakua na ulazima wa kupiga dawa hizo, basi dawa zipigwe wakati wa jioni ambapo shughuli za uchavushaji zitakua zinaishilia.

Hali ya Hewa Inahathiri kikubwa sana Utengenezaji wa matunda ya Tikiti maji:

Wakati wa msimu wa mvua na msimu wa baridi, uchavushaji na utengenezaji wa matunda unapungua sana kutokana na kwamba nyuki wakati huo wanakua hawafanyi kazi (inactive)

Wakati wa mvua pia, poleni huoshwa na mvua, hivyo kupelekea matunda yenye muundo usiofaa (misshapen fruits). Hizo ndio sababu kuu kwanini uzalishaji wa matikiti kipindi cha mvua au kipindi cha baridi hupelekea mavuno duni.

Umwagiliaji pia unaathiri kiasi cha matunda yatakayotengenezwa. Aina ya umwagiliaji itaamua kiasi cha maua ambayo mwishowe yatakomaa. Mfano umwagiliaji wa njia ya mvua (sprinkler irrigation) hupelekea kuoshwa kwa poleni kwenye maua. Njia nzuri zaidi ya umwagiliaji wa tikiti ni umwagiliaji wa matone (drip irrigation), mfumo huu wa umwagiliaji tutakuja kujifunza siku za mbeleni.

Shughuli za shamba pia huweza kuathiri uchavushaji wa matikiti, hii inajumuisha palizi na upigaji dawa.

Kila mmea wa tikiti shambani unahitaji umakini (attention) kama vile uko peke yake shamba zima

Tengeneza ratiba yako ya upandaji ili kuepuka msimu wa mvua kipindi cha utoaji wa maua. Yaani kipindi cha utoaji wa maua kisikutane na msimu wa mvua.

Kuelewa mfumo wa uchavushaji wa matikiti na ukizingatia hayo tuliyojifunza hapo juu unaweza kuongeza uzalishaji hadi asilimia themanini (80%), maana hii itaamua idadi ya matunda na ubora wake.

+255627109810

Comments