AZAM FC YAINYOA TENA SIMBA LIGI KUU


Kipigo cha pili mfululizo ndani ya mwezi mmoja Simba wanapewa na Azam, baada ya Januari 13 kufungwa pia 1-0 katika fainali ya Kombe la Mapinduzi

Goli pekee lililowekwa kimiani na nahodha John Raphael Bocco ‘Adebayor’ limetosha kuipa Azam FC ushindi wa 1-0 dhidi ya Simba SC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


Bocco alifunga bao hilo dakika ya 70 baada ya kupata mpira mrefu wa mshambuliaji Mghana Mohammed Yahya na kumhadaa beki kisiki wa Simba, Mzimbabwe Method Mwanjali kabla ya kumchambua kipa Mghana, Daniel Agyei. 

Hicho kinakuwa kipigo cha pili mfululizo ndani ya mwezi mmoja Simba wanapewa na Azam, baada ya Januari 13 kufungwa pia 1-0 katika fainali ya Kombe la Mapinduzi Uwanja wa Amaan, Zanzibar, bao pekee la Himid Mao. 

Kipigo hicho kinapunguza matumaini ya ubingwa kwa Simba SC, iliyouanza vizuri msimu, kwani ikibaki na pointi zake 45 za baada ya kucheza mechi 20 inaweza kuenguliwa kileleni na Yanga ikiifunga Mwadui Uwanja wa Taifa.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi Erick Onoka aliyesaidiwa na washika kibendera Hassan Zani, wote wa Arusha na Josephat Masija wa Mwanza, dakika 45 za kipindi cha kwanza zilishuhudiwa timu zote zikicheza kwa kujihami zaidi.

Makocha wote Mcameroon Joseph Marius Omog na Mromania Aristica Cioaba walianzisha mshambuliaji mmoja mmoja katika vikosi vyao, upande wa Azam Nahodha John Bocco na Simba, Juma Luizio.

Kulikuwa na viungo wengi kwa timu zote, upande wa Azam wakianzishwa, Mcameroon Stephan Kingue, Himid Mao, Joseph Mahundi, Frank Domayo na Ramadhani Singano ‘Messi’ na Simba wakianzishwa Jonas Mkude, Said Ndemla, Jamal Mnyate, Muzamil Yassin na Pastory Athanas.

Kwa sababu hiyo haikuwa ajabu timu zote kumaliza dakika 45 zikiwa zimemiliki sawa mpira, ingawa tu hakukuwa na mashambulizi ya kusisimua.

Kipindi cha pili, makocha wote wakaamua kufunguka kwa kuingiza washambuliaji zaidi wakitoa mabeki na viungo. 

Mabadiliko hayo yalifanya mchezo uanze kuwa mtamu kutokana na kushambuliana kwa zamu.

Hata hivyo, ilikuwa ni bahati yao Azam FC baada ya kosa kosa za pande zote mbili kwa muda mrefu, Nahodha Bocco akafunga dakika ya 70.

Bocco mwenye bahati ya kufunga dhidi ya vigogo Simba na Yanga, alifunga bao hilo pekee dakika ya 70.

Baada ya kuruhusu bao hilo, Simba wakafunguka zaidi kusaka bao la kusawazisha kwa kusukuma mashambulizi mfululizo langoni mwa Azam.

Lakini safu ya ulinzi ya Azam ikiongozwa na ‘beki mbabe’, Aggrey Morris ilisimama imara kudhibiti mashambulizi yote ya Simba

Comments

Popular posts from this blog

KILIMO CHA TIKITI MAJI( WATER MELONY)