Jela miaka 7 kwa kujeruhi kwa panga
MFANYAKAZI wa Kiwanda cha Jambo Plastic, Mustapha Juma (35) amehukumiwa kifungo cha miaka saba jela na kufanya kazi ngumu, baada ya kupatikana na hatia ya kumjeruhi kwa panga Elias Charles na kumsababishia maumivu makali Juma, ambaye ni Mkazi wa Kurasini Dar es Salaam, alihukumiwa kifungo hicho jana katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala mbele ya Hakimu Mkazi John Msafiri.
Hakimu Msafiri alisema ameridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka uliokuwa na mashahidi wanne.
Alisema kuwa mshitakiwa huyo pamoja na kifungo chake, atatakiwa kufanya kazi ngumu kwa kuwa alimjeruhi mlalamikaji sehemu mbalimbali za mwili wake hususan kwenye kitovu na kumsababishia maumivu.
Katika utetezi wake juu ya kwa nini asipewe adhabu kali, Juma, alidai kuwa ana familia inayomtegemea na hivyo kuiomba Mahakama hiyo kumpunguzia adhabu maombi ambayo yalitupiliwa mbali na mahakama hiyo.
Inadaiwa kuwa Desemba 14, 2014 maeneo ya Vingunguti ndani ya Wilaya ya Ilala Dar es Salaam, mshitakiwa akiwa na panga alimjeruhi sehemu mbalimbali za mwili ikiwamo kitovuni mlalamikaji, Charles na kumsababishia maumivu makali kinyume cha sheria.
Katika hatua nyingine, mahakama hiyo imemhukumu kutumikia kifungo cha miaka minne jela au kulipa faini Sh milioni moja itakayoenda sambamba na fidia ya Sh milioni 20, Vishal Pandia(33) raia wa India baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa fedha Sh milioni 20.
Comments
Post a Comment