Simba, Yanga jino kwa jino


Simba

Yanga

MBIO za ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara zimeendelea kuwa za farasi wawili, Simba na Yanga baada ya matokeo ya katikati ya wiki.

Jumanne Yanga ilipata ushindi wa ugenini wa 1-0 dhidi ya wenyeji Maji Maji kwenye Uwanja wa Maji Maji mjini Songea na kuvunja mwiko wa kutoshinda dhidi ya timu hiyo kwenye uwanja huo kwa miaka 30.

Wakati Yanga wakipata ushindi huo muhimu, Simba ililazimishwa suluhu na wenyeji Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, kabla ya usiku wake Azam na wao kulazimishwa suluhu ya nyumbani na Mbeya City.

Baada ya matokeo hayo, Simba inaendelea kuongoza kwenye msimamo wa Ligi Kuu, ingawa sasa ni kwa pointi mbili zaidi kutoka pointi nne dhidi ya Yanga kabla ya michezo hiyo.

Simba wana pointi 45 na mabingwa watetezi, Yanga wana pointi 43 wakati Azam wamefikisha pointi 31 baada ya wote kucheza mechi 19.

Simba inayofundishwa na Mcameroon Joseph Omog inataka taji la kwanza la Ligi Kuu tangu mwaka 2012, lakini ili kutimiza lengo hilo inapaswa kuendelea kupambana kubaki kileleni mpaka mwishoni mwa msimu.

Yanga imekuwa na mwendo wa kusuasua msimu huu, lakini Simba imeshindwa kutumia fursa hiyo vizuri kwa kuhakikisha inajikusanyia pointi zaidi na kusogea mbali.

Ilitarajiwa baada ya Yanga kushinda 1-0 Songea Jumanne, Simba nayo ingeshinda Morogoro juzi na kuendelea kuwazidi kwa pointi nne mahasimu wao hao, lakini matokeo yake ikadondosha pointi mbili.

Vinara hao sasa wanakabiliwa na mchezo mgumu mbele yao dhidi ya Azam Januari 28 ambao utarudisha kumbukumbu ya mchezo wa fainali ya kombe la Mapinduzi uliochezwa Januari 13 mwaka huu mjini Zanzibar.

Simba watakuwa kwenye presha zaidi kwa kutambua kama itashindwa kuibuka na ushindi dhidi ya Azam, na Yanga ikafanikiwa kushinda mchezo wao dhidi ya Mwadui utakaochezwa siku moja baada ya Simba basi rasmi Simba itaenguliwa kileleni mwa msimamo.

Mechi zinazofuata baada ya hapo zitazishuhudia Simba ikisafiri mpaka Songea kuumana na Majimaji Februari 4 na siku moja baadae Yanga itawakaribisha Stand United kwenye uwanja wa Uhuru.


Comments

Popular posts from this blog

KILIMO CHA TIKITI MAJI( WATER MELONY)