SHIRIKISHO la Soka nchini (TFF) limesema Uwanja wa kumbukumbu ya Namfua hauna vigezo
SHIRIKISHO la Soka nchini (TFF) limesema Uwanja wa kumbukumbu ya Namfua ulioko mkoani hapa hauna vigezo vya kutumika katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Salum Madadi, alitoa kauli hiyo juzi alipokuwa akiukagua uwanja huo kwa lengo la kutoa maelekezo ya marekebisho yanayotakiwa kufanyika ili timu ya Singida United iliyopanda daraja iweze kuutumia.
Madadi alisema ili uwanja huo uweze kutumika katika ligi hiyo ya juu nchini, itawalazimu wamiliki kuchukua vipimo upya na ushauri wa kiufundi wa matengenezo yanayohitajika ili wafanye ukarabati na kufikia viwango.
“Lakini kubwa zaidi sehemu yenyewe ya kuchezea inahitaji kuboreshwa haraka na kuwekwa uzio kwa ndani, pia kuna haja ya kuwa na vyumba vya kubadilishia,” alisema Madadi.
Katibu Msaidizi wa CCM Singida, Adamu Makulilo, alisema kuwa anaamini kwa kuunganisha nguvu za wadau wa soka mkoani hapa watakamilisha matengenezo yaliyoelezwa na hatimaye Singida United ikautumia katika mechi zake za nyumbani za Ligi Kuu.
“Naamini baada ya kuunganisha nguvu za Wanasingida, klabu pamoja na wanachama tunaweza kutekeleza na kukamilisha kasoro zilizoelezwa na ifikapo Oktoba, tunategemea mambo yatakuwa yamekamilika,” alisisitiza katibu huyo.
Naye Abdurahman Sima, Katibu Mkuu wa Singida United alisema kuwa itakuwa ni aibu kwa mkoa endapo kituo hicho kitahamishwa, jambo ambalo litawakatisha tamaa wadau wa soka waliochangia kuisaidia timu hiyo kupanda daraja
Comments
Post a Comment